Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Hassan Kabeke ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya Maulidi ya Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) Mkoa wa Mwanza, iliyoandaliwa na Sheikh Hashim Ramadhani, ambapo alizungumzia kwa kina historia ya kuenea kwa Uislamu katika maeneo ya Tanzania na mchango wa makundi mbalimbali katika historia hiyo.
Katika hotuba yake, Sheikh Kabeke alieleza kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa walioeneza dini ya Uislamu katika kipindi hicho, hata kabla ya Tanganyika kuundwa kama eneo la kisiasa lililokuja kujulikana baadaye, walikuwa Wafursi wenye asili ya Kishirazi. Alisema baadaye walifuatiwa na Washihiri kutoka Yemen, na kisha Wamanga kutoka Oman, ambao nao walishiriki katika historia ya kuenea kwa Uislamu katika eneo hilo.
Akiendelea kueleza historia hiyo, Sheikh Kabeke alimtaja miongoni mwa masheikh waliofika katika zama hizo kuwa ni Sheikh Khalfani bin Muhammad Zindi Jaali, ambaye alisema alikuwa na asili ya Kiajemi kutoka Shirazi. Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke, Sheikh Khalfani alifika miaka ya 1871 na alifariki mwaka 1925, huku kaburi lake likiwa katika eneo la Kabondo, Kigoma, ambako watu wameendelea kulizuru. Sheikh Kabeke aliongeza kuwa mwaka uliopita uliadhimishwa ukumbusho wa miaka 100 tangia kifo chake.
Sheikh Kabeke pia alisisitiza umuhimu wa elimu na utafiti wa historia katika kujenga uelewa sahihi miongoni mwa Waislamu, akisema kuwa wakati mwingine anapomsikia mtu akiwatukana Mashia, jambo hilo linaweza kuonyesha kwamba bado hajawa na uelewa mpana wa kielimu kuhusu historia na nafasi ya makundi mbalimbali katika historia ya Uislamu. Alisema Waajemi wa Kishirazi walikuwepo Tanganyika kwa muda mrefu kabla ya Tanganyika kuwa Tanganyika, ambapo walijenga misikiti, wakaswalisha Waislamu na kuwafundisha dini, huku akisema athari zao zinaonekana hadi maeneo ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Akizungumzia changamoto ya kutunza historia, Sheikh Kabeke alisema; tatizo kubwa miongoni mwa Waislamu ni kutopenda kuandika na kuhifadhi historia za masheikh na viongozi wao wa dini. Alisema hali hiyo ni tofauti kwa baadhi ya maeneo ya Pwani, kama Tanga, ambako kuna juhudi za kuandika na kuhifadhi historia ya masheikh na matukio ya kidini yaliyotokea katika maeneo hayo.
Kwa upande mwingine, Sheikh Hassan Kabeke aligusia pia historia ya Maulidi nchini Tanzania, akirejea maandiko ya Dkt. David Livingstone, ambaye kwa mujibu wa maelezo yake, mwaka 1871 alipofika Ujiji, Kigoma, alimkuta Sheikh Mwinyi Kheri bin Mwinyi Mkuu akiwa tayari ameanzisha Zawiya ya Qadiriyya kwa takribani miaka 40. Kwa mujibu wa hoja hiyo, Zawiya hiyo ilianzishwa karibu mwaka 1831, jambo ambalo Sheikh Kabeke alilitumia kueleza kuwa shughuli za Maulidi zilikuwa tayari zikiendelea katika maeneo hayo tangia kipindi hicho.
Akihitimisha hotuba yake, Sheikh Kabeke alisema kuwa: Uwepo wake katika hafla hiyo ya Maulidi ya Mashia ulikuwa na malengo mawili; kwanza, kuungana na ndugu zake Waislamu wa Kishia, na pili, kuufahamisha umma kuwa tofauti za madhehebu hazipaswi kuondoa msingi wa umoja wa Kiislamu.
Maoni yako